shetani wa Kitanzania

14:25:00 Unknown 0 Comments




MTU mmoja alifariki na kwenda jehanamu. Kufika huko akakuta kuna jehanamu tofauti tofauti kwa kila nchi. Akaamua kuzunguka zunguka ili aweze kuipata jehanamu yenye maumivu kidogo zaidi.

Akaiendea jehanamu ya Ujerumani. Akamwuliza mtu aliyemkuta mlangoni. "Wanakufanyaje ukiingia humu?"

Akajibiwa. "Kwanza wanakuweka kwenye kiti cha umeme kwa saa moja, kisha wanakulaza kwenye kitanda cha mizumari kwa saa moja nyingine. Kisha anakuja shetani wa Kijerumani anakucharaza bakora kutwa nzima."

Mtu huyo hakuipenda kabisa jehanamu hiyo. Akaamua kujaribu jehanamu za Marekani, Uingereza, Urusi na nyinginezo nyingi. Lakini akagundua kuwa zote zina adhabu sawa tu na jehanamu ya Ujerumani.

Kisha akaifikia jehanamu ya Tanzania. Akastaajabu kuona kuna foleni ndefu kweli ya watu wakisubiri kuingia humo. Kwa mshangao usiosemekana akauliza, "Jamani kwani humu wanawafanyaje?"

Akajibiwa, "Kwanza wanakuweka kwenye kiti cha umeme kwa saa moja, kisha wanakulaza kwenye kitanda cha mizumari kwa saa moja nyingine. Kisha anakuja shetani wa Kitanzania anakucharaza bakora kutwa nzima."

Akazidi kustaajabu. Akauliza, "Lakini mbona kinachofanyika humu ni sawa kabisa na kinachofanyika kwenye jehanamu zingine, sasa kwa nini hapa kuna foleni kubwa sana watu wote wanakimbilia huku?"

Jamaa mmoja akamshika mkono. Akamvutia pembeni. Akamnong'oneza, "Watu wanakimbilia huku kwa kuwa jehanamu ya Tanzania haina umeme wa uhakika, unakatika katika kila dakika kwa hiyo kiti cha umeme hakifanyi kazi. Halafu pia misumari ilishalipiwa lakini wala haijaletwa na mzabuni kwa hiyo kitanda cha humu ni raha tu kukilalia. Na jambo jingine ni kuwa shetani wa Kitanzania alipokuwa duniani alikuwa mtumishi wa umma. Kwa hiyo ameshazowea kufika ofisini na kusaini kitabu cha mahudhurio na kisha kuondoka zake kwenda kufanya shughuli zake binafsi."

You Might Also Like

0 comments: