Ujanja ujanja wamtokea puani mzee wa mjini

21:38:00 Unknown 0 Comments




Fundi ujenzi mmoja ambaye alifanya kazi kwa muda wa miaka mingi katika kampuni moja ya ujenzi, alihitaji kupumzika (kustaafu) kwani alishafikia umri wa kustaafu.

Alimfuata mkurugenzi wa kampuni yake na kumwambia mkakati wake wa kuiacha nyumba ya kampuni kwani alihitaji kustaafu na kurudi kijijini kwake, akaishi na mkewe pamoja na familia yake kubwa yenye wajukuu wengi na vitukuu. Mzee alijua angekosa sana fursa ya kupata fedha ila kwa ajili ya umri wake alihitaji kupumzika.

Mkurugenzi wake alihuzunika sana kwani alijua anampoteza mtu aliyefanya kazi kwa ukweli na kujituma kwa miaka mingi.Lakini akamwomba yule mzee amfanyie msaada mmoja tu kabla hajastaafu rasmi.

Mkurugenzi akamwomba yule mzee amjengee nyumba moja ya mwisho na baada ya hapo atamruhusu astaafu.
Mzee alikubali ingawa moyoni alihuzunika kwani alishachoka,basi akachukua vifaa duni na watu wazembe wazembe (wasio makini) ili wamsaidie haraka amalize ile kazi kwa kulipua na aondoke zake . Binafsi aliona ingefaa ili aachane na ile kazi kabisa kwa kulipua kwani asingeweza kuitwa tena. 

Baada ya kumaliza kazi kwa miezi michache yule mzee akamwambia mkurugenzi wake na mkurugenzi alikuja na alipofika pale akachukua funguo na kuufungua mlango mkuu na akamwambia, " Kuanzia leo hii ni nyumba yako, Na hii ni zawadi yangu kwako kwa kuwa mfanyakazi wangu kwa muda mrefu” 

Yule mzee alipatwa na mshangao pamoja na aibu kuu, kwani kama angejua alikuwa akijenga nyumba yake mwenyewe angeifanya kuwa bora na ya kuvutia na asingetumia vile vifaa duni na wasaidizi wasio makini.

Hivyo ndivyo wengi wetu tufanyavyo mambo katika maisha yetu ya kila siku, ni wepesi wa kulaumu, kupiga kelele na hata wavivu kuliko tunavyojituma.

Hatujitumi kwa asilimia kubwa makazini mwetu ila niwepesi wa kushangazwa na matokeo yetu na kuilaumu dunia kuwa tunaonewa wakati ni hali tulizozitengeneza wenyewe. Lakini kama tungejua mapema ni rahisi kwa sisi kubadilika na kupata matokeo mazuri

Hebu jifananishe na mzee huyu, fikiri kuhusu nyumba, kisha fikiria je wewe una jenga nyumba (Maisha) ya aina gani? Je unajenga kwa busara au ni kama mzee wetu?

Kumbuka unahitaji kujituma katika kila ulifanyalo kwa manufaa yako ya baadae. Kwani kila ulifanyalo sasa ndio mafanikio yako ya kesho….. Ishi kwa malengo

You Might Also Like

0 comments: