TAHADHARI...HUU NDIO UGONJWA UTOKANAO NA KUZAMA CHUMVINI (MAPENZI KWA NJIA YA MDOMO, NI CHANZO KIKUU CHA SARATANI YA KOO.)
Saratani imeendelea kuwa tishio hapa nchini
huku hofu ikiendelea kuikumba jamii
kutokana na wataalamu wa afya kushindwa
kufahamu tiba halisi ya maradhi hayo hatari.
Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean
Road zinaonyesha ongezeko la saratani ya
mdomo na koo kwa kiasi kikubwa kutoka
kesi 167 mwaka 2006 hadi 277 mwaka 2012.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga
Ocean road, Julius Mwaiselage anaeleza kuwa
watanzania wasipende kuiga mambo ambayo
si sahihi bila kujua madhara yake kama
kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo.
“Saratani ya mdomo ipo, na nyingine
zinasababishwa na zinaa “ anasema Dk
Mwaiselage
Tafiti za saratani
Tafiti mbalimbali zimewahi kufanyika nchini
na kubaini kuwepo kwa ongezeko la saratani
ya mdomo.Utafiti uliofanywa na Dk Innocent
Mosha wa Kitengo cha Patholojia cha
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
umebaini aina za saratani 1,594, kati ya hizo
509 zikiwa ni za midomo kwa mwaka 2003
pekee.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kati
ya saratani 509 za mdomo, saratani 242
zilisababishwa na Virusi vya Human Papiloma
ambavyo hutokana na zinaa. “Ninachojua
mimi ni kuwa Virusi vya HPV husababishwa
na magonjwa ya zinaa, hivyo mtu anayeugua
saratani ya aina hiyo, imetokana na zinaa,”
anasema Dk Mosha.
Wanaume waathirika zaidi wa Saratani
Takwimu hizo ni zile zilizopatikana kwa watu
waliokwenda kufanyiwa uchunguzi katika
Mkoa wa Dar es Salaam pekee. Dk Mosha
anasema kuwa wanaume ndiyo huathiriwa
zaidi na saratani ya mdomo ambapo kwa
hapa nchini, asilimia 53 ya wanaume
waliofika MNH kwa ajili ya vipimo,
walibainika kuugua saratani hiyo, huku
wanawake wakiwa ni asilimia 47. Utafiti
kama huo ulifanywa pia na Dk Amos
Mwakigonja, mkuu wa Idara ya Patholojia
katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili
(MUHAS).
Dk Mwakigonja alifanya utafiti wa saratani ya
mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma ambapo
wagonjwa 78 walibainika na saratani hiyo
kuanzia mwaka 1990 hadi 2003. “Saratani za
mdomo zipo za aina nyingi na zimetofautiana
kulingana na visababishi vyake,” anasema Dk
Mwakigonja. Katika utafiti wake Dk
Mwakigonja alibaini kuwa wanawake wengi
walikuwa na saratani ya mdomo aina ya
Kaposi’s Sarcoma kuliko wanaume.
Hata hivyo, utafiti huo ulionyesha kuwa
asilimia 50 ya wanaume walikuwa na saratani
ya mdomo hatari zaidi (systemic) kuliko
wanawake ambao ni asilimia 37.
Mapenzi kwa mdomo husababisha maradhi
Dk Mwakigonja anasema kuwa mapenzi
yoyote kwa njia ya mdomo lazima
yasababishe maradhi ya zinaa iwapo mmoja
ameambukizwa. Pia anasema kwamba
sampuli nyingi za wanaume wanaojihusisha
na mapenzi na wanaume wenzao (mashoga)
zilibainika na saratani ya mdomo. Utafiti huo
ni sehemu ya utafiti wa Shahada ya Uzamivu
ambao ulionyesha kuwa wagonjwa wengi wa
saratani ya mdomo walikuwa ni wanaume
wenye umri wa miaka kati ya 38 na
kuendelea na wanawake ni 31.
Ufatiti wa WHO Tanzania
Shirika la Afya Duniani (WHO) pia lilifanya
utafiti mwaka 2010 nchini kwa kushirikiana
na Kituo cha Taarifa za HPV, ambapo
ilibainika kuwa asilimia 20 ya saratani za koo
na mdomo nchini zinasababishwa na ufanyaji
wa mapenzi kwa njia ya mdomo.
Taarifa hizo za WHO zinaeleza kuwa wanaume
747 hugundulika na saratani ya mdomo kila
mwaka wakati wanawake 472 hubainika na
saratani hiyo pia. Wakati huohuo, wanaume
wanaopoteza maisha kutokana na saratani
hiyo ni 444, kwa mwaka na wanawake ni 270,
kwa mwaka. Utafiti wa WHO umebaini kuwa
saratani ya mdomo inashika nafasi ya sita
katika aina 24 za saratani 24 zinazoisumbua
zaidi Tanzania.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wanaume
wanaoathirika zaidi ni wenye umri wa kati ya
miaka 15 na 55, ambao tayari wameshaanza
kujihusisha na ngono. Kama maradhi
mengine ya kuambukiza, Virusi vya HPV
huambukizwa kwa urahisi zaidi kutoka kwa
wanawake kwenda kwa wanaume kuliko
kutoka kwa wanaume kwenda kwa
wanawake. Utafiti huo uliodhaminiwa na
mfuko wa Bill na Melinda Gates na Kituo cha
Saratani na Mpango wa Utafiti wa Taasisi ya
ICO unaeleza kuwa mitandao ya kijamii na
picha za ngono ndiyo chanzo cha watu wengi
kuiga ufanyaji wa mapenzi ya aina hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la The New York
Times, tafiti zimefanyika na kubaini kuwa
asilimia 70 ya wagonjwa wanaobainika na
saratani ya koo na mdomo duniani,
husababishwa na Virusi vya Human
Pappiloma vinavyotokana na magonjwa ya
zinaa.Tafiti hizo zinaonyesha kuwa wagonjwa
wengi wanaogundulika na saratani hiyo ni
wanaume wenye umri wa kati, wenye uwezo
wa kifedha, wasiovuta sigara wala siyo
walevi waliokubuhu.
Utafiti huo ulibaini kuwa wanaume wapo
hatarini zaidi kupata saratani ya koo
inayosababishwa na Virusi vya HPV. Miaka ya
80, idadi ndogo ya watu waliougua saratani
ya koo walihusishwa na maambukizi ya Virusi
vya HPV. Kihistoria, watu waliobainika na
ugonjwa huo, ni wenye umri wa miaka 70
kwenda juu ambao walikuwa ni wale walevi
waliokubuhu na wavuta sigara.
Ilielezwa kuwa Virusi vya HPV vipo kwa wingi
kiasi ambacho watu wazima wanaojihusisha
na ngono ya aina yeyote ile, huweza kupata
maambukizi ya zinaa hata kama siyo saratani.
Hata hivyo ilibainishwa kuwa saratani
isababishwayo na virusi vya HPV ni rahisi
kuitibu kuliko saratani ya koo isababishwayo
na tumbaku au pombe kali.
Virusi vya HPV ni nini?
Kwa jina la jumla, saratani ya koo au mdomo
huitwa saratani ya kichwa na shingo. (Neck
and Head Cancer) HPV ni miongoni mwa
virusi hatari zaidi duniani visababishwavyo na
magonjwa ya zinaa na vinaweza kuathiri
sehemu mbalimbali za mwili. Zipo aina zaidi
ya 120 za HPV, baadhi huweza kuzalisha
usugu (warts) ambazo si saratani katika
sehemu za siri, mikononi na miguuni.
Maambukizi ya HPV hufanyika kwa urahisi,
hata kwa kugusana ngozi au majimaji, huku
maambukizi mengine yakisababishwa na
ngono.
Virusi hatari na vinavyosababisha saratani ni
HPV-16, HPV-18, HPV-31 na HPV 45. Aina hii
ya Virusi vya HPV husababisha saratani
ambapo uvimbe waweza kujitokeza kwa
ndani na unaweza usionekane ukilinganisha
na vivimbe vingine vya saratani. Wataalamu
wanasema HPV-16 na HPV-18 inahusishwa
zaidi na saratani ya shingo ya kizazi na
endapo mapenzi kwa njia ya mdomo
yatafanywa na mtu mwenye uambukizo huu
ni rahisi kuambukizwa.
Share kama umeelewa
Source: remmymwemablog
0 comments: