Kama una dalili hizi, basi jua kwamba hujiamini…!

07:22:00 Unknown 0 Comments


1. Kugusika kirahisi:
Mtu asiyejiamini huwa anagusika kirahisi sana, jambo dogo linaweza
kumnyima furaha kwa kiwango kikubwa.
Jambo dogo linaweza kumuudhi kupindukia. Kuna watu ambao kwa utani mdogo sana wa kawaida wanakasirika sana, wanajihisi vibaya na kuumia sana.

2. Kuwategemea wengine kuthibitisha:
mtu asiyejiamini siku zote haamini kuhusu uwezo
wake, maamuzi yake au hisia zake, hadi athibitishiwe na wengine kwanza.
Hata kama anajua jambo, ana kipaji, hawezi kuamini katika uwezo na nguvu hizo hadi watu
wengine wamthibitishie kuhusu usahihi na ubora huo.

3. Kujilinganisha katika kufanya mambo au thamani:
Wengi tunakabiliwa na kutojiamini
kwenye eneo hili. Tunajilinganisha sana na wengine. Tunafanya mambo yetu mengi wa
kushindana na kujilinganisha kuliko kufanya kwa ajili yetu na kwa viwango vyetu.
Unanunua gari, siyo kwa sababu unahitaji gari, bali kwa sababu fulani amenunua gari, unataka kumuoneshea. Kila unachofanya ni
kwa sababu ya wengine, siyo kwa sababu yako.

4. Kujishusha na kujipandisha thamani kuliko wengine:
Kuringa na na kutamba ni dalili ya
kutojiamini na sio kujiamini, kama wengine wanavyodhani.
Mtu anayeringa na kujikweza sana anajaribu kupunguza maumivu ya hisia zake zilizo chini kuhusu thamani yake.
Hii ni sawa na kujishusha. Mtu anajishusha kwa sababu anaamini kwa kujishusha watu watamwona ni wa maana na anayestahili.
Lakini bado kujishusha maana yake ni kutafuta huruma na kukubaliwa na wengine, kutokana na hisia za kuwa mtupu. Mtu anayejishusha na yule anayejikweza wote ni
mtu mmoja, bali wenye pande mbili tofauti.
Kujikweza na kujishusha ni jambo lile lile kwa sura mbili tofauti.

5. Kutaka kuwafurahisha wengine kwa gharama, hasara yake:

Asiyejiamini yuko tayari kuumia, lakini awafurahishe wengine, yaani
wengine wamuone kuwa wa maana au wasimshushe.
Mtu anatakiwa kulipa mchango
wa tukio fulani, yaweza kuwa mchango wa harusi au harambee ya kuchangia jambo fulani ambapo kiwango kilichopangwa labda ni
shilingi 20,000 tu. Lakini mtu huyu anaweza kusimama na kutangaza kutoa mchango mkubwa kupita kiasi kilichopangwa wakati
fedha hizo hana, ili tu kujionyesha kwamba na yeye anazo.
Mwisho wa siku anaingia kukopa na kulipa fedha hizo kwa maumivu makubwa sana. Angeweza kulipa kiwango alicho nacho au hata kama hana kuwa mkweli. Hapana,
anataka wengine wamuone wa maana, lakini kwa gharama inayompa maumivu makubwa
sana. Mifano ni mingi, lakini huu mmoja nadhani unakupa picha nazungumzia watu wa namna gani.

6. Kuogopa kuwajibika na kutupia wengine mizigo:
Wengi tuna udhaifu huu. Mtu
asiyejiamini, hayuko tayari kuwajibika, kwani kuwajibika kunamfanya ahisi kushuka. Kwa
hiyo ili asishuke, hata akikosea, atajitahidi kusingizia au kuwatupia wengine lawama.
Hata kwenye kosa la wazi kabisa, ataanza kutafuta kosa dogo hata la mwaka juzi na kulitumia
kosa hilo, kujisafisha. Hebu kagua kwenye uhusiano, hasa kwenye ndoa utaona sana udhaifu huu ukijitokeza.
Mpenzi au mke anabeba mimba, mwanaume anakuwa wa
kwanza kulaumu, “Wewe kazi yako kuzaa zaa tu kama panya.” Mwanaume anaweza kusema
kwa kejeli na kulaumu. Hayuko tayari kuwajibika kwamba, hata yeye ana mchango katika jambo hilo. Kwake yeye mwanamke
ndiye mwenye makosa.

7. Kutumia nguvu nyingi kulinda hadhi ya uongo: Kuna watu ambao wanaazima magari, wanaazima nguo na vitu vingine ili waonekane
kuwa watu wa maana. Hufanya hivyo kwa matumizi ya nguvu nyingi kiakili, kihisia na kimwili ili wajionyeshe. Kuna idadi kubwa ya
watu ambao hulinda hadhi za uongo kwa lengo la kutaka kuonesha kwamba, wana
thamani. Hii kwa kawaida, ni tabia ambayo inatokana na kutojiamini.

8. Kuogopa sana au kutokuwa tayari kukosolewa, lakini kupenda sana kukosoa:
Mtu asiyejiamini anaogopa na kuchukia sana kukosolewa. Ukimkosoa, bila kujali kama ni
kwa njia ya kujenga au kubomoa, hatakubali.
Mtu asiye jiamini ana kawaida ya kujihami sana, ili asionekane au kujulikana kuwa hajui au hawezi. Kwa hiyo, kumkosoa ni sawa na
kumtia msumari wa moto kwenye kidonda. Ili sasa asionekane kuwa hajui, ili udhaifu wake usionekane, anakuwa na kawaida ya kuwakosoa wengine. Anataka wengine
waonekane kuwa hawawezi,hawana nguvu,hawastahili na mwengine yanayofanana na hayo.
Lengo lake ni kuwashusha hao wengine,akiamini kuwa, hiyo itampandisha yeye.

9. Aibu za ziada na kushindwa kutazama watu usoni:
Mara nyingi aibu ni dalili ya mtu
kushindwa kujiamini. Aibu maana yake ni kwamba, mtu anaamini na kuhisi kama vile wengine wana mashine za x-ray kiasi kwamba,
wanawaona hadi tumboni.
Kwa kutojiamini, mtu anahisi kama vile, kila anachofanya kinaonwa na kufanyiwa tathmini, hivyo anaogopa atakosea na kila mtu atajua.
Hiyo hasa ndiyo maana ya aibu. Aibu nyingine ni matokeo ya mtu kuamini kwamba, hana thamani, ukilinganisha na wale watu alionao.
Hivyo, kwa kuhisi hana thamani, hujiona kama yuko chini mbele ya wale anaoamini kuwa wanathamni zaidi.

10. Kutawaliwa na majuto ya jana na hofu za kesho:
watu wasiojiamini wamejaa majuto ya siku za nyuma na wamesheheni hofu za maisha yao ya baadaye. Ni mara chache kwa mtu asiyejiamini kuishi maisha ya leoleo.
Kama hajuti kuhusu maisha yake yaliyopita, basi atakuwa amejaa hofu za maisha yake ya kesho.

You Might Also Like

0 comments: