Maajabu haya....Mungu tupe ujasiri
Nusu saa kabla ya kwenda kanisani kuhudhuria ibada ya mkesha wa X-Mas akikuja bibi mmoja ambaye sijawahi kumwona maishani.
Bibi huyu aliomba tumsaidie chakula na kuwa pia angependa ajumuike nasi katika ibada ya
mkesha na kuwa amefanya hivyo kwani siku hiyo alikosa magari ya kurudi kijijini kwao kwani hakuwa na nauli.
Nikaingia chumbani na mke wangu na kumwambia,tutafanyaje kuokoa jahazi hilo?
Kwani X-MAS hii imekuja wakati ambao kwanza maisha yametubana sana na mambo mengine ndani ya nyumba ni siri yetu jinsi tuishivyo.
Kwa moyo mmoja tukakubali kumpa akiba yetu ya 30,000 kama nauli ya kumpeleka mpaka kijijini kwake na pia tukajumuika wote katika ibada ya usiku ule.
Tulishangazwa na jinsi bibi yule bibi alivyokuwa mchangamfu na mwenye kutushauri jinsi ya kuwa na busara na ushirikiano katika kuijenga familia bora.
Zaidi alijigusia suala la kutokata tama wala kutegemea kulipwa fadhila kila unapotoa msaada.
Wakati anaondoka siku ya pili yaani leo asubuhi akanipa zawadi ya kitambaa kizuri chenye maua
na mke wangu akapewa mtandio.
Zawadi hizi zikanikumbusha maumivu niliyoyapata mwaka mmoja uliopita siku kama ya
leo nipofiwa na dada mmoja ambaye nilikutana nae akiomba msaada wa fedha za kutibiwa
saratani ya matiti.
Na baada ya vita ngumu ya kuupigania uhai wake alikufa mikononi mwangu na kuniachia
mwanae mmoja niwe baba mlezi na zawadi kama alizoniachia bibi huyu.
Zawadi hizi na kumbukumbu hii zilinifanya nilie kwa uchungu nikimkimbuka dada yule na baada
ya fikra hizo nikapitiwa na usingizi kabla ya mke wangu kuniamsha na kuniambia nina mgeni.
Mgeni huyu kaja kunipa taarifa ya kuanza kazi rasmi january 19 mwakani.
Kazi hii mimi na mke wangu tumeipigania tangu mwaka jana na mpaka sasa naamini ni Mungu
ananipa mafanikio kupitia dada yule aliyenifia mikononi mwangu.
Mungu awabariki wote mnaofanya matendo mema kwa watu wote, na mzidi kupata baraka kila siku kwa kadri mwombavyo.
0 comments: