NI LINI HASA UNAWEZA KUSEMA NDOA HII SASA BASI!!??
Hakuna kipimo hasa kwa sababu kila mmoja anaguswa kwa namna tofauti na jambo fulani, lakini kila mmoja wetu ana kiwango tofauti cha kuwavumilia na hata kuwasamehe wengine. Watu wengi huwa wanajiuliza wanapokosewa na wenzao kwenye ndoa, ‘sijui nimwache au nimpe tena nafasi?’
Dini zetu nazo zinasisitiza kusameheana,na hata mila na desturi zetu. Lakini kusisitizwa na kutenda ni vitu au mambo mawili tofauti. Bado dini hizo hizo [binafsi ni muislam ila nimeona vyema kuyatazama haya kote] kuna makosa ya kindoa ambayo zinayatazama kama makosa yenye kusameheka, lakini ambayo hayaruhusu au kutoa nafasi kubwa kwa ndoa kuendelea.
Moja ya makosa hayo ni uzinzi, yaani kutoka nje ya ndoa. Kutoka nje ya ndoa ni kosa ambalo limechangia katika kuvunja ndoa nyingi sana. Hata hivyo, kwa bahati mbaya imetokea kuvunja ndoa pale ambapo zaidi anayefumaniwa ni mwanamke. Mtu anapozini tunasema hampendi mwenzake. Hii ina ukweli kidogo kwa sababu kuzini kunafanywa kwa sababu ambazo ni tofauti kutoka moja hadi nyingine.
Kwa hiyo inashauriwa kwamba ndoa inaweza kuvunjwa au ni vizuri ikavunjwa kama inahusisha kuzini. Hata hivyo kama ni kuzini ambako[wapo wanaoshauri] kumetokea mara moja, inabidi mtu atafute sababu kwa nini kulitokea. Kama atathibitisha kwamba mazingira yaliyopelekea kuzini huko yalikuwa na ugumu katika kuepukwa, mume au mke wa huyo aliyefumania inabidi ajaribu kutoa nafasi kwa mwenzake. Kama kuzini ni mara kwa mara, haishauriwi ndoa kuendelea kuwepo.
Mtu anapoishi kwenye ndoa ambayo imegubikwa na uzinzi, anajiweka kwenye hatari nyingi sana. Kwa siku hizi, hatari ya kwanza ni maradhi. Lakini kuna hatari nyingine kadhaa. Kuishi na mzinzi ni kuishi katika kero kihisia. Wenye wake au waume ambao ni walevi, mara nyingi pia wanakabiliwa na maradhi yasiyoonekana hospitalini kwa sababu ya kujiumiza kihisia.
Kosa lingine ambalo linapotokea, mtu anatakiwa kufanya uamuzi wa kuifikisha ndoa tamati ni ulevi. Kama mme au mke ni mlevi sugu, hatua ya awali ni kwa mume au mke huyo kujitahidi kumsaidia mwenzake.
Hilo linaposhindikana, kuna haja ya kufikia mahali ambapo talaka ndio njia muafaka.
Ulevi sugu una maana ya mtu kuthamini pombe kuliko kitu kingine na hivyo kunywa karibu muda wote, hata ule muda ambapo mtu yuko shughulini. Hii ina maana pia kwamba, mtu huyo hatajali kuhusu mke wala watoto. Lakini ulevi sugu huwafanya wengine kuwa wakorofi, kuwa wazinzi, kufuja fedha na kuingia kwenye maradhi kirahisi.
Jambo lingine ambalo linapojitokeza kwenye ndoa, mtu anashauriwa kuvunja ndoa hiyo ni ufujaji. Mara nyingi wanaofuja ni wanaume, ingawa wanawake wapo pia kwa kiasi kidogo. Kufuja kurudia tena na tena kumuumiza mpenzi kwa makusudi kwa kauli au vitendo.
Inaweza kuwa ni kwa kashfa, kusimanga, kubeza, kutukana kuhusu mtu au familia alimotoka ama kuhusu uwezo na pia mwonekano wake. ‘Wewe mwanamke gani, wakiitwa wanawake nawe utakwenda kweli.’ Ni baadhi tu ya kashfa. Kuna kupiga, kusukuma, kusukasuka, kulazmisha tendo la ndoa na matumizi mengine ya nguvu.
Vitendo hivi vinaporudiwa mara kadhaa kwa lengo la kumfanya mwingine ahisi vibaya na kumfanya anayetenda ajihisi mshindi, huku ndiko kufuja. Mara nyingi ushauri wa ndoa za namna hii ni mwanamke kuondoka.
Ushauri huu hutolewa haraka kwa sababu, ni vigumu kwa mfujaji kukubali kwamba anafuja na kusaidiwa kutoka humo. Pale ambapo mfuaji anakubali kwamba hiyo ni kasoro na yuko tayari kusaidiwa, hakuna haja kwa mwanamke kuamua kuvunja ndoa. Lakini pale ambapo mfujaji hakubali kwamba ana matatizo, ndoa hii ni kifo cha moja kwa moja.
Jambo lingine ambalo linachukuliwa kama kigezo halali cha ndoa kuvunjwa ni mume au mke kufanya mapenzi na mtoto wake. Kuendelea kuishi kwenye ndoa baada ya jambo kama hili kutokea ni kujidanganya. Baada ya tukio kama hili, hisia za wahusika hufungwa na uhusiano kwa njia zote hukwama. Watu wanaweza kukaa kama mke na mume lakini kweli ni kwamba, mmoja atakuwa anaumia kwa saa 24 za siku.
Jambo lingine ni jaribio lolote la mume au mke kutaka kumdhuru mwingine kimwili. Kuna wakati mume a mke anaweza kufanya jaribio la kutoa maisha ya mwenzake iwe ni kwa kumpiga au kumwekea sumu au chochote.
Jambo jengine nalo ni kauli halisi kutoka kwa mpenzi. Mke au mume anaweza kumwambia mwenzake kwamba, hamtaki au hampendi tena. Inapofikia hali kama hii, inabidi aliyejulishwa aulize vizuri kama mwenzake anasema hayo kwa dhati. Aliyesema anaposema ni kwa dhati, inabidi mhusika asubiri tena kauli hiyo kwa mara ya pili.
Anapotamka kauli hio kwa mara ya pili, inabidi aliyeambiwa aulize tena, na aliyeitamka akisema ni kwa dhati , mhusika inabidi asubiri kwa mara ya mwisho. Kauli ya ‘sikutaki tena’ au ‘nimeshasema sikuhitaji’ inaporudiwa kwa mara ya tatu, hapo ni lazima uamuzi ufanywe.
Mpenzi anapokwambia kwamba hakutaki mara tatu, huna sababu ya kujipendekeza, kwa sababu wewe ni binadamu kamili kama yeye. kujipendekeza kuna maana ya wewe kuwa dhaifu kwake na hivyo kujiumiza na kujishusha bure.
Kumbuka kama mume au mke amethubutu kukutamkia mara tatu kwamba hakutaki uking’ang’ania kuishi naye, ni lazima atakudhuru. Kumbuka hakutaki na tusichokitaka huwa tunakiondoa kwa njia yoyote tunayomudu kutumia.
0 comments: