Siku kiherehere changu cha kumaliza kreti la ndovu kilivyogeuka na kuwa somo zito....Ni aibu tupu

11:10:00 Unknown 0 Comments

Siku moja wakati wa sherehe kama tuliyonayo sasa nikiwa chuoni kuna rafiki yangu mmoja mwenye asili ya America akanialika kwenda kumtembelea shambani kwake.

Rafiki yangu yeye alikuwa mkulima na mfugaji na muda wake mwingi aliutumia shambani akisimamia mifugo na mazao yake.

Kama ujuavyo kuwa wenzetu linapokuja suala la kujituma katika majukumu yao basi wao huwa hawana mchezo zaidi ya kukazana kuweka kazi zao sawa na mipangilio yao.

Basi nilialikwa niende pale na marafiki zangu ninaowajali sana wawili na kufanya idadi yetu kuwa watatu. Tukaanza safari na hatimaye tukafika pale tukiwa salama.

Kwa kuwa siku hiyo ilikuwa ni siku ya mapumziko na aliniomba niwahi sana kufika pale ikiwezekana asubuhi sana basi mimi nikawahi pale nikiwa na marafiki zangu mida kama ya saa mbili na nusu asubuhi nikawa pale.

Tukakuta mwenyeji wetu alishaamka na yuko kwenye mazizi yake ya mifugo akikagua. Haraka baada ya kutuona akatufuata na hata tulipotaka kujaribu kumsaidia kazi akagoma kwani siku ile alipenda tukae na kuongea hasa tujadili maisha na kuburudika.

Wakati huo mpishi wake alishatuita twende tukapate kifungua kinywa na amini usiamini kwa maisha ya kichuo ambayo wajua tena boom halikuwa likieleweka sana na hata lilipotoka bado liliisha kwa muda mfupi kutokana na matumizi mabovu na maisha kuwa ya kuunga unga lakini bado hatukukosa cha kusingizia mpaka wengine walidai ile hela ina mashetani na ndio maana haidumu.

Hivyo siku hiyo nikapania kula ipasavyo yaani bila kukwepesha macho.... breakfast ilikuwa ya kutisha hivyo tukaila kistaarabu sana hasa ukizingatia ule ugeni bado ulitutawala na vijiaibu.

Baada ya breakfast akatuita nje na kutuuliza tulitaka kula nini kwa ajili ya chakula cha mchana na jioni? Of-course kuku lilikuwa chaguo letu na akaongeza kuwa tungependelea kuku wa aina gani.... Kubanikwa lilikuwa chaguo namba mbili kwani tulishaulizwa kila mtu angependelea kinywaji gani.

Nusu saa baadae mfanyakazi wake akawa karudi pale akiwa na kreti moja moja kwa kila mtu aliyechagua kinywaji fulani...Mie wa ndovu nikawa nimewekewa kreti langu na akasema hayo hapo ni yenu kazi kwenu naye akafunguliwa chupa yake ya wine.

Tukawa tunafungua bia moja moja huku tukiendelea kujadili maisha ya chuo na maisha baada ya chuo huku kila mmoja wetu akionesha matumaini na imani ya kuwa na kazi nzuri baada ya kuhitimu chuo na kulalamikia maisha ya chuo yalivyo magumu sana.

Mpaka tunaitwa kwenda kupata chakula cha mchana iadadi ya chupa cha bia zilizokwisha nyweka ilikuwa imepanda panda na tumechangamka vya kutosha.

Mezani kila mtu pia alipewa kuku mzima kabisa aliyebanikwa na kuwekwa makorokoro kibao na kutuambia tule kila mtu kuku wake naye mweneji wetu akawa na kuku nwake na pale kwenye chakula tulikuwa wanne tu yaani mimi marafiki zangu wawili pamoja na mwenyeji wetu.

Kulikuwa na kimya cha dakika kadhaa kila mtu akiwa busy kumchambua kuku wake na mimi nilikuwa wa kwanza kunyanyua uso juu nikiwa namalizia kuutafuna mfupa wa mwisho wa yule kuku.

Sekunjde chache baadae na jamaa zangu wakawa wamemaliza na tukanyanyuka na mwenyeji wetu kwenda kwenye eneo letu la bia. Ila mwenyeji wetu hakuwa mlaji sana yeye alikata sehemu ndogo tu ya yule kuku akamla na kumrudisha jikoni yule mwingine aliyebaki na sisi kilichofanikiwa kurudishwa jikoni ilikuwa ni kachumbali na matunda kidogo.

Maongezi yaliendelea wakati huo yeye alikuwa yupo na glas yake ya wine na chupa haikuonekana kushuka sana, moyoni nikawa naona jamaa sio mwanywaji ngoja sisi kazi tuzionyeshe. 

Pamoja na maongezi yale pia tulikuwa na michezo tuliyoicheza pale na katika kitu nilichokipenda ni ule muda wa kwenda kuvua samaki kwenye moja ya mabwawa yake. Ki ukweli vijimazoezi vile vilitukwa vikisaidia sana pombe kutopanda kichwani na kama miujiza inafika saa kumi na mbili na nusu za jioni nilibakiwa na bia 3 tuu kati ya lile kreti.

Na muda huo chakula tukawa tumeitwa tena kwa chakula cha jioni na tulipoingia mle ndani mezani kukawekwa vile tulivyoviacha mchana yaani kachumbari na matunda machache tuu na mwenyeji wetu akapashiwa kuku wake ana kukata kipande kidogo na kula pale nasi tukawa tunasubiri chakula hakiji tukaishia kula kachumbari ile pamoja na pilipili kali na kisha tukanyanyuka kuelekea kwenye eneo letu la vinywaji.

Muda huo mimi nilibakiwa na bia kidogo kwenye glas na jamaaa zangu mmoja alishamaliza bia zake na mmoja alibakiwa na bia tano na mwenyeji wetu akawa yupo na glas yake ya wine na chupa ikiwa bado inaonyesha uhai.

Mimi nikanyanyuka ili niende kuchukua bia moja kutoka kwenye kreti la jamaa yangu yule mwenyeji akanikataza na kusema acha kwani zako ziko wapi? Nikamjibu mzee zimeisha...

Ndio hapo akatuuliza sasa ni kwa nini pia jioni hii  mmekula kachumbali pekee?

Jamaa yangu akadakia naona wapishi walitusahau kwenye ratiba....

Na kwa nini mmeamua kunywa bia zote siku moja na yule kuku kumla kwa mlo mmoja?

Nikajibu mzee hizi bahati huwa haziji mara mbili hivyo ukizingatia na mambo haya kuwa adimu kwenye maisha yetu ya chuo hivyo ukiipata bahati itumie ilivyo.

Mzee akatuambia, na hii ndio hali halisi ya maisha yenu na msipojirekebisha itawawia vigumu kuyamudu maisha mara baada ya kuhitimu chuo.

Yule kuku alipoletwa mimi nilikata kidogo na kumwifadhi mwingine na ndio maana jioni hii nimeweza kumla mwingine na amebaki ambaye kesho pia nitaweza kumla.

Hivyo hivyo mimi kinywaji nilichojichagulia nimeweza kukinywa taratibu na nimebakiwa na kiasi kikubwa ambacho naweza kunywa kesho na keshokutwa pia.

Maisha ni sawa na mfano huu bahati huja mara moja katika kila jambo na unapofikiwa na bahati hiyo unatakiwa kutengeneza mazingira ya neema hiyo kudumu kwani maisha hayaishi siku moja.

Kama utapata kiasi kikubwa cha fedha leo ni kutokana na nidhamu yako ya kutumia itakufanya udumu na fedha hizo na kuongezeka.

Katika kila ufanyacho kumbuka akiba ya kesho la sivyo utayaona maisha hayana nia nzuri nawe.... Alimaliza kuongea nasi tukaaga kurudi makwetu nyuso zikiwa na aibu.......






You Might Also Like

0 comments: