Sababu 10 za kwa nini wafanyakazi wazuri wanaikimbia kampuni yako

21:25:00 Unknown 0 Comments


Na Fadhy Mtanga
Unaweza ukawa una taasisi nzuri, ama tuseme kampuni nzuri kweli. Unajitahidi kutafuta wafanyakazi wazuri. Wanaweza kuwa wale waliofanya vizuri zaidi mashuleni. Ama, wale wenye uzoefu mkubwa katika kada husika. Wanaweza kuwa wabunifu wa kiwango cha juu. Wanaweza kuwa na weledi wa aina yake. Unapata timu ya wafanyakazi wenye kujituma. Wenye jitihada za kiwango cha juu.

Lakini, ghafla bin vuu, wafanyakazi hao wanaanza kupukutika katika kampuni yako.
Unajikuta unaanza kukimbiwa na mfanyakazi mmoja baada ya mwingine. Unaanza kujishika kichwa ukijiuliza maswali. Mkosi gani tena huu? Kwa nini wafanyakazi waikimbie kampuni yako? Ama, hata wale ambao hawajaikimbia, mbona wamepunguza morali ya kazi. Mbona hawana furaha?

Wabobefu wa mahusiano kazini wanasema, zipo sababu nyingi zinazochangia kwa kiasi kikubwa, wafanyakazi kuikimbia kampuni yako.

Katika sababu nyingi zilizopo, hizi 10 ni sehemu ya sababu hizo.

Sababu ya Kwanza

Huwafundishi mameneja wako namna ya kuhusiana na wafanyakazi wa chini yao
Kwamba, eti kwa sababu meneja wako amekuwa akifanya kazi vizuri basi unaamini anaweza kuwaongoza wengine. Kama kampuni, ni vema uhakikishe unawapatia
mafunzo mameneja wako mara kwa mara kwa minajili ya kuboresha mahusiano yao na wafanyakazi wanaowaongoza.
Wafanyakazi wanaoongozwa na mameneja wa ovyo hukata tamaa ya kuendelea kufanya kazi katika kampuni yako. Wakipata upenyo, lazima watakukimbia.
Sababu ya Pili
Huwapi wafanyakazi wako mrejesho
Kwa kuwa kampuni ni yako, basi unaona wacha mambo yaende kadri ya unavyotaka wewe. Wafanyakazi wako wanajituma kufanya hili na lile, lakini hutaki kuwapa mrejesho juu ya kile wanachokifanya. Hali hiyo huwavunja moyo wafanyakazi wako.
Asilimia 79 ya wafanyakazi hupenda kupewa mrejesho kwa wakati kuhusiana na jambo lolote linalogusa maisha yao na utendaji wao katika kampuni yako.
Sababu ya Tatu
Huzipi kipaumbele takwimu sahihi kutoka kwa wafanyakazi wako
Kama, kila kitu unajua wewe, wala hutaki kutumia takwimu halisi katika ufanyaji maamuzi unadhani ni mfanyakazi gani ataona hapo ni pahala stahiki kwake?
Sababu ya Nne
Kila kitu unakifanya siri
Siri gizani? Kila mambo katika kampuni yako unayafanya kwa siri. Unataka kuongeza mapato kwa asilimia kadhaa – siri. Unataka kampuni yako ikuwe kwa
asilimia fulani – siri.
Wafanyakazi hawapendi kuendelea kuwepo katika kampuni yenye kila-kitu-siri.
Wafanyakazi wanapata hamasa ya kuendelea kuifanyia kazi kampuni yako endapo watashirikishwa malengo ya kampuni. Hii inawafanya wajione kuwa wanacho kitu cha kukichangia katika kampuni yako. Ukificha kila jambo, wao wanajiona hawahitajiki.
Mishahara haijatoka, wewe unafanya siri. Hutaki kuwaambia kwa nini imechelewa. Wao wanatazama tu kalenda. Wanaona zinafika tarehe 40, 50, 60 ama hata 70 wewe kimya tu ukijitia kutingwa na mambo yako.
Ama hakika, watachapa lapa.
Sababu ya Tano
Huwashirikishi kuhusiana na mustakabali wa kampuni yako
Kila mtu anakuwa kivyake. Mameneja wanafanya hivi, ilhali wafanyakazi
wanafanya vile. Hawachezi wimbo mmoja katika kufikia malengo ya kampuni yako.
Ukitaka wafanyakazi waendelee kubaki katika kampuni yako, wafanye wajione ni sehemu ya malengo ya kampuni yako. Vinginevyo, utaishia kukimbiwa kila siku.
Sababu ya Sita
Hufanyi tathimini ya ushiriki wa wafanyakazi wako
Wewe una kampuni, lakini hufahamu namna wafanyakazi wako wanashiriki katika yaihusuyo kampuni yako. Huna utaratibu wa kuyasikiliza kwa uzingatifu maoni ya wafanyakazi wako.
Waulize wafanyakazi waliopo. Wakwambie, kwa nini mwaka uliopita wafanyakazi kadhaa waliacha kazi? Wape nafasi wakupe maoni, kwa nini utendaji wao unaporomoka?
Sababu ya Saba
Hutaki kuweka mkakati wa ushirikishwaji wa wafanyakazi wako
Unafahamu kuwa hakuna ushirikishwaji wa wafanyakazi katika mambo yaihusuyo kampuni yako. Lakini bado, hutaki kuandaa mpango mkakati wa kuhakikisha unaongeza ushirikeli kwa wafanyakazi wako.
Tafiti kadha wa kadha zinasema, makampuni ambayo kuna mikakati kabambe ya ushirikishwaji wa wafanyakazi huongeza tija kwa asilimia 78 na faida kwa
asilimia 40. Pia, wafanyakazi wanaoshirikishwa vizuri huongeza ufanisi wao kwa asilimia 20.
Vinginevyo, utaishia kuajiri wafanyakazi wapya kila siku.
Sababu ya Nane
Hutaki kuwawajibisha mameneja wabovu
Mambo yanakwenda bora-liende. Kuna watu wanavurunda katika kampuni yako,
nawe unabaki kimya. Hutaki kuchukua hatua stahiki. Kitendo hicho huwavunja
moyo wafanyakazi wenye mapenzi mema ya kutimiza madhumuni ya kampuni yako.
Weka kanuni za nidhamu katika kampuni yako. Yeyote anayezikiuka kanuni hizo awajibishwe sambamba na matakwa ya kanuni. Hii itawafanya wale wafanyakazi makini wazidi kuzielekeza nguvu zao katika kuifanikisha azma
ya kampuni yako.
Lakini ukiyaacha mambo shaghalabhaghala, wale wafanyakazi makini watakukimbia.
Sababu ya Tisa
Unaendekeza majibizano mabaya na wafanyakazi wako
Sawa, mfanyakazi amefanya kosa, kwa nini umsemee mbovu? Kuwa meneja wa kampuni, zipo stadi za kuhusiana na wafanyakazi wako katika nyakati mbalimbali. Mfanyakazi mwingine hakosei akiwa na dhamira mbaya. Jifunze lugha nzuri ya kimeneja.
Usilumbane na wafanyakazi unaowaongoza. Watakuona huna maana. Wakikuona huna maana, kampuni yako haitokuwa na maana tena kwako. Nini kinafuata,
wenye weledi wao, watashika hamsini zao.
Sababu ya Kumi
Hutaki kuwathamini
Wewe ndiyo wewe. Bosi, meneja, mkurugeniz, Afisa Mkuu na majina yote makubwa yako. Unawaona wafanyakazi wa chini yako kama vinyangarika tu. Hutaki kuthamini kazi wanazokufanyia. Unawadharau. Huna muda wa kuwasikiliza matatizo yao. Hujali lolote.
Unawaona wao ndiyo wenye shida sana ndiyo maana wanafanya kazi kwako. Umeliwa!
Nani anapenda kufanya kazi mahali anapopuuzwa?
Tafiti zinasema kuwa asilimia 80 ya wafanyakazi wanasema kuthaminiwa kwao mahala pa kazi, ndiyo hamasa kubwa kwa wao kufanya kazi vizuri zaidi.
Waheshimu wafanyakazi wako. Waoneshe kuwa unakithamini kila wanachokifanya kwenye kampuni yako. Wape pongezi kila inapobidi.
Kwa kumalizia
Usidhani mshahara ndiyo kila kitu katika kampuni yako. Lakini kumbuka pia, siyo kila mwenye uwezo wa kuwa na kampuni, ana uwezo wa kuiongoza. Weka timu nzuri ili kuiongoza kampuni yako.
Usijisahau ukadhani kila mfanyakazi anatiwa hamasa na mshahara unaompa katika kampuni yako. Usipate kiburi.
Kwa nini ukimbiwe na wafanyakazi katika kampuni yako wakati hayo hapo juu yanaepukika? Ifanye kampuni yako iwe pahala ambako kila mfanyakazi anatamani kupafanyia kazi.
Fadhy Mtanga ni mshairi, mwandishi wa riwaya na mjasiriamali. Vile vile, ni mshauri wa masuala ya mahusiano kazini akibobea katika usuluhishi wa migogoro mahali pa kazi.

You Might Also Like

0 comments: