MAKOSA MAKUBWA AMBAYO WENGI HUYAFANYA KATIKA UHUSIANO, YAJUE UBADILIKE

06:19:00 Unknown 0 Comments

MAISHA ni kama picha ambayo unaijenga
kwenye fikra zako. Haya ni maneno ambayo
niliyaeleza kwenye makala haya katika sehemu
iliyotangulia wiki iliyopita. Endapo utawaza
mema na kutamani kumfanyia mwenzi wako
vitu vizuri, ni rahisi kutekeleza.
Utakosea mno, kama utakuwa unasumbuliwa
na mawazo kwamba unachokitenda, mpenzi
wako naye atakaa na kufikiria kisha akutendee
kama unavyomfanyia.
Kwa miaka kadhaa, nimejifunza kujua tabia za
watu kwenye mapenzi na kubwa ambalo
nimebaini ni kwamba saikolojia ya ndani ndiyo
ambayo inaleta utata.
Uhusiano wa wengi unashindwa kudumu kwa
sababu hiyo. Ukweli ni kwamba ndani ya mtu,
kunakuwa na matarajio ambayo hayafikiriwi
upande wa pili.
Hili ni tatizo lakini linaweza kuwa kinyume
chake kama mhusika ataligundua hilo na
kulitafutia ufumbuzi. Kwa nini uwaze peke
yako? Iweje kichwa kiume kwa tamaa ya
kutekelezewa jambo ambalo linaweza kuingizwa
kwenye majadiliano? Mapenzi ni kitu
kinachokutanisha nafsi mbili zenye hisia tofauti,
kwa hiyo inabidi kuelewana ili muende sawa.
Acha kuwaza peke yako. Mshirikishe mwenzako
jinsi ambavyo wewe ungefurahi kwa namna
atakavyohusika kwenye mapenzi yenu.
Muelekeze cha kufanya. Mshauri muonekano
ambao wewe utakupa nguvu ya kujiamini
kwamba upo kwenye uhusiano salama.
Usipojadiliana naye, unadhani utasaidiwa na
nani?
Kosa kubwa ambalo watu wengi huwa
wanafanya ni kuwaacha wapenzi wao na
kwenda kujadiliana na marafiki. Mtu anaweza
kuketi na rafiki yake na kumwagia lawama
chungu nzima jinsi asivyofurahishwa na mwenzi
wake, wakati angezungumza na mhusika
mafanikio yangeonekana kwa urahisi zaidi.
Achana na tabia ya kumsengenya mwenzi wako
kwa marafiki zako. Unamponda kwa yale
anayofanya kwa kuona hayapo sawa lakini
mapenzi hayapo hivyo. Tambua kwamba wewe
pekee ndiye mwenye nafasi ya kumfanya
mpenzi wako abadilike kulingana na jinsi
unavyotaka. Jijengee mawazo chanya kuanzia
leo.
Binadamu walivyo katika jinsi mbili tofauti,
ndivyo wanavyotofautishwa na namna ya
kupenda pia jinsi ya kuhusika kwenye mapenzi.
Wengi huishi na maumivu kwa kuona kwamba
anachowaza, hakipo kwa mwenzi wake.
Mathalan, unapenda mpenzi wako akununulie
zawadi, hilo lirekebishe kwa kumuelekeza kwa
upole.
Mwambie: “Mpenzi wangu, napenda sana ile
simu.” Zungumza hivyo halafu ukae kimya.
Naye akili inafanya kazi, kwa hiyo kama uwezo
unaruhusu atakununulia. Jiepushe na tabia ya
kuomba jamvi msibani. Pengine hana lakini
wewe unalaumu kuwa hakujali ndiyo maana
hajakununulia.
Kosa lingine kubwa ambalo wengi hulifanya ni
kufananisha uhusiano wa watu wengine na
kutaka kulazimisha uhusika wao ufanane na
wenu. Mfano; mtu anaona jinsi rafiki yake
anavyotendewa na mpenzi wake, kwa hiyo naye
anatamani iwe hivyo. Ni binadamu wawili
tofauti, ni ngumu kuwa na tabia za kufanana.
Uvumilivu unahitajika.
KUKOSEA TAFSIRI
Binadamu kila mmoja kwa namna yake, anayo
njia ya kuonesha ishara za mapenzi. Hata hivyo,
ipo wazi kuwa wengi hufanana pale
wanapochachawa kutokana na kuzidiwa na
hisia za kupenda. Kila mmoja anaruhusiwa
kupenda lakini pupa zikikuzidi, ni rahisi
kuonekana mapepe. Haipendezi kuonekana
hivyo.
Ieleweke kuwa ipo jamii ya watu ambao
wanaweza kupenda lakini wasioneshe waziwazi
hisia zao. Wakakomaa kisabuni, wewe ukadhani
hawapendi kumbe wanaumia ndani ya nyoyo
zao. Hili likae kichwani kwako, usije ukafanya
kosa kubwa la kukosea tafsiri, matokeo yake
uhusiano wako ukakaa tenge.
Tambua pia kuwa ipo jamii ambayo inaweza
kuonesha waziwazi kwamba wanapenda kumbe
hakuna lolote. Ni uchangamfu tu uliopo ndani
yao. Anaweza akawa anakujali, ukiwa mbali
anakupigia simu. Ukiwa na tatizo anajitoa
kukusaidia lakini hiyo siyo ishara kuwa
anakuhitaji kimapenzi. Ni mambo ya urafiki tu
hayo.
Hivyo basi, kabla hujaingia kwenye uhusiano
wa kimapenzi, hakikisha huchanganyi mambo.
Usimtafsiri mtu kwa alama za juujuu. Fanyia
kazi kile unachohisi. Usije ukachukia kwamba
mtu unayempenda anakuchukia, wakati kumbe
mwenzako ndiyo swaga zake. Lazima aweke
madoido kidogo kwa kuhofia kuonekana
mwepesi.
Wala usije ukadandia mti ambao siyo kwa
kudhani unapendwa, wakati mwenzako ni
geresha tu! Chukua hatua sahihi, kabidhi moyo
wako kwa yule anayekupenda, si kwa sababu
akikuona anakuchekea na kujishaua, la hasha!
Kaa kwa yule ambaye amedhihirisha mapenzi
ya kweli kwako. Ukikosea tafsiri, utaumia mbele
ya safari.
KUTARAJI UHUSIANO UKUPE FURAHA PEKEE
Ni vizuri kutaraji furaha kwenye uhusiano
wako, kwani ndivyo inavyotakiwa. Kosa
linalojitokeza hapo ni kuwa wahusika huwa
hawapigi mahesabu ya changamoto ambazo
hujitokeza. Ni vizuri kuyabeba mapenzi katika
sura halisi kwa maana zipo siku ambazo
hutafurahi. Ni changamoto.
Tatizo ni kwamba kila mmoja anapoyatafakari
mapenzi, huwaza kuwa mpenzi wake ndiye
atayabadilisha maisha yake na kumfanya awe
na furaha. Hata siku moja hawezi kwenda
mbele na kuutesa ubongo wake, akiwaza na
kuwazua jinsi ambayo yeye anaweza kufanya ili
kumpa furaha na amani mwenzi wake.
Angalau wanaume wachache hufikiria mema
kwa ajili ya wapenzi wao lakini kwa wanawake
tafiti zinaonesha kwamba asilimia 98 ya
wanawake kabla ya kuingia kwenye uhusiano,
husumbuliwa na ubinafsi kwa sababu huwaza
mambo ambayo wao watafanyiwa na wapenzi
wao na siyo wao kuwafanyia.
Kwa kuweka hoja zote kwenye kapu moja, ni
vizuri kila mmoja akawekeza furaha yake kwa
mwenzi wake. Ni makosa makubwa kutegemea
matunda ambayo hujafanya jitihada zozote
kuyapanda na kuyastawisha.

You Might Also Like

0 comments: