Sababu Kumi Kwa Nini Ni Muhimu Wewe Kuwa na Blog Yako Leo.
Blog ni sehemu ndogo ya mtandao wa internet
ambapo unaweza kuweka maoni au maandiko
yako na yakaonekana dunia nzima. Tofauti na
website(tovuti), blog ni rahisi kuanzisha, rahisi
kuendesha na haihitaji gharama kubwa,
unaweza kuendesha bure kabisa. Kuna faida
nyingi sana za wewe kuwa na blog, katika
makala, tengeneza blog yako leo na upate faida
hizi tano niliongelea faida za kiuchumi za kuwa
na blog. Leo nitaongelea faida za maendeleo
yako binafsi kwa kuwa na blog yako. Hapa
nazungumzia blog za kuandika mambo yenye
msaada kwa watu wengine na sio za kuripoti
habari za udaku.
Hizi hapa ni sababu kumi kwa nini ni muhimu
wewe kuanzisha blog yako leo hii na sasa hivi;
1. Kuendesha blog ni changamoto na
changamoto zinakufanya ukue.
Wote tunajua kwamba bila ya changamoto
huwezi kukua kiakili na kimawazo. Unapokuwa
na blog na kujiwekea ratiba ya kuandika kwenye
blog yako kuna wakati inakuwa vigumu kabisa
kwako kuweza kuandika kitu chenye maana.
Lakini kama utaweza kukaa chini na kuandika
hata kama hujisikii kuandika inakujengea
nidhamu kubwa na utaweza kufanya mambo
mengine makubwa kwenye maisha yako.
2. Kujifunza mambo mapya.
Kuwa na blog ni sehemu nzuri sana ya kujifunza
mambo mazuri tena kwa bure kabisa. Kwanza
kabisa utajifunza kuandika kitu ambacho
kitakusaidia sana kwenye shughuli zako. Pili
utajifunza zaidi kuhusu mada unazopendelea
kuandika. Kwa njia hii utajua mengi zaidi na
yatakusaidia kwenye kazi na biashara zako.
3. Kuleta tofauti kwenye maisha ya watu.
Chochote utakachoandika kwenye blog yako
ambacho kinakusaidia wewe, jua kuna mtu
mwingine pia akikisoma kitamsaidia sana. Kwa
kuandika mambo ambayo yanawasaidia watu na
wakakutafuta kukushukuru kwa maandiko yako
inakupa moyo na kukufanya uandike zaidi. Hii
imekuwa ikitokea kwangu karibu kila siku.
4. Unakuwa mtaalamu.
Unapokuwa na blog na ukachagua mada fulani
ukawa unaziandikia mara kwa mara itakufanya
wewe kuwa mtaalamu wa mada hizo, na
baadae watu watakufuata kwa ushauri. Kwa
mfano kama una blog na unaandika kuhusu
kilimo na ufugaji watu watakapokuona ukiandika
kwa muda mrefu inakuwa rahisi kwao kukufata
na kutaka ushauri zaidi kuhusiana na mambo
hayo. Kwa njia hii unaweza kutengeneza
biashara nzuri baadae.
5. Unayaweka mawazo yako kwenye mtandao
mkubwa.
Kwa kuwa na blog iliyounganishwa na mitandao
ya kijamii ni rahisi kwa watu kusambaza ujumbe
wako kwenye mitandao yao. Kama unaandika
vitu vyenye msaada kwenye maisha ya watu ni
rahisi kwao kuwashirikisha wengine. Hii itakuza
sana blog yako na itatengeneza fursa ya
biashara baadae.
6. Kujenga uzoefu mpya.
Kama umeajiriwa na kazi yako haina hamasa
kubwa ni rahisi sana kuwa na msongo wa
mawazo. Ila kama ukiwa na blog yako unakuwa
na uzoefu mpya ambapo utakuwa na utaratibu
wa kujifunza zaidi, kuandika na kushirikisha
dunia mawazo yako. Pia itakuwa rahisi kwako
kujadiliana na wasomaji wako kuhusu mada
mbalimbali. Hivyo badala ya kutumia internet
yako au ya ofisi kwa kuangalia mambo yasiyo na
maana kwenye mtandao, hebu anzisha blog
yako leo na uanze kufurahia maisha yako.
7. Kukutana na watu wapya.
Kwa kuwa na blog inayoandika mambo mazuri
inakuwa rahisi sana kwako kukutana na watu
wapya na wa muhimu sana kwenye mada
unazoandika na hata biashara. Kupitia blog
nimeweza kukutana na watu wengi sana ambao
mpaka sasa tunashirikiana kibiashara na katika
mambo mengine muhimu ya maendeleo.
8. Kuandika kuhusu maisha yako.
Kuwa na blog sio lazima uandike mada kwa ajili
ya watu wengine. Unaweza kuwa na blog
utakayoandika safari ya maisha yako. Uzuri ni
kwamba unaweza kuifanya blog kuwa private
hivyo ukaiona wewe tu au watu utakaowaruhusu
waione.
9. Kukabiliana na hofu zako.
Blog ni njia moja nzuri sana ya kukabiliana na
hofu zako. Kama una hofu ya kupingwa hivyo
unashindwa kutoa maoni yako kwenye vikao
muhimu anzisha blog yako leo. Mada yoyote
utakayoandika kwenye blog yako lazima kuna
mtu atakupinga, kwa njia hii utajifunza
kukabiliana na upinzani wa aina hii na moja kwa
moja unaondoa hofu ya kupingwa. Moja ya
makala nilizokuwa naandika mwanzoni kabisa
wakati naanzisha AMKA MTANZANIA ni umuhimu
wa watu kujisomea vitabu ili kujiendeleza
binafsi. Nilipata upinzani mkubwa sana kutoka
kwa baadhi ya watu kama vile niliwashikia
fimbo na kuwalazimisha. Iliniumiza sana
mwanzoni lakini baadae nilijifunza ni sehemu ya
uandishi.
10. Kutengeneza fursa za kibiashara.
Kuwa na blog ni njia rahisi ya kutengeneza fursa
mpya za biashara. Unaweza kutafutwa kutokana
na utaalamu wako kwenye mada unayoandika
na kuwa mshauri mzuri. Unaweza kuuza bidhaa
zako zinazotokana na mada unayoandika kupitia
blog yako. Kuna fursa nyingi za kibiashara
utazipata kwa kuwa na blog.
Kama mpaka sasa huna blog anzisha blog yako
leo. Sahau chochote kuhusu biashara au
kutengeneza fedha kupitia blog hiyo. Anza kwa
kutengeneza utaalamu wako kupitia mada
unayochagua kuandika, baadae fedha
zitakufuata zenyewe.
Nimependezwa na makala yako ndugu yangu..✊!! Kuna kitu nimejifunza ambacho nilikuwa Sina hapo awali.
ReplyDelete