HITAJI LA MUHUMU KULIKO YOTE.
Kijana fulani alikwenda kwa mzee mmoja kujifunza hekima. Kijana huyo alikuwa amedhamiria sana kuwa mtu mwenye hekima na upeo wa hali ya juu ili hatimaeaweze kuwa kiongozi wa nchi yake.
Bila shaka kijana aliamua kwenda kwa mzee huyo na si mwingine baada ya kusikia sifa kwamba huyo alikuwa ndie mwalimu bora na anae heshimika zaidi katika kufundisha hekima. Baada ya mahojiano na taratibu zote kumalizika, kijana alikubaliwa kuanza mafunzo maalum ya hekima.
Miaka mingi baadae kijana akaamini kwamba amekwishapata hekima ya kutosha na akamuomba mwalimu wake amruhusu kuondoka. Mzee huyo akamwambia yule kijana kwamba atamruhusu kuondoka endapo atafaulu mtihani atakaompa; na hivyo akamtaka ajiandae kuufanya mtihani huo katika kipindi cha siku tatu.
Siku tatu baadae mzee akamkalisha kijana kwenye kiti na kumpatia karatasi ya mtihani. Kijana alipoangalia karatasi hiyo akakutana na swali moja tu, 'andika vitu ambavyo binadamu akiwanavyo atajiona kuwa maisha yake yamekamilika'.
Kwa vile kijana alikuwa ameishapata hekima ya kutosha kwa haraka sana akaandika
orodha ya vitu alivyoamini kwamba ni vya muhimu sana na kumpelekea orodha hiyo mzee. Orodha hiyo ilijumuisha vitu vifuatavyo:
(a) Afya,
(b) Uzuri,
(c) Mali,
(d) Kupendwa,
(e) Usalama,
(f) Umaarufu.
Mzee alipoiona orodha hiyo alitabasamu na kukaa katika kiti kilichokuwa pembeni ya kijana. Akamwambia " mwanangu umefanya kazi nzuri sana na ninakupongeza kwa hekima uliyona" baada ya hapo akachukua peni na kuanza kusahihisha mtihani ule huku akichambua kipengele kimoja baada ya kingine.
Akasema 'afya' ni kitu cha muhimu sana kwa maana bila kuwa na afya bora huwezi kuishi vizuri wala kuwa na furaha. Na ndio maana mtu huwa tayari kuuza vyote alivyo navyo ili apate matibabu ya kumpa afya njema.
Uzuri una sehemu yake muhimu ingawa uzuri unatofautiana kati ya mtu na mtu; hata hivyo,uzuri kila mtu anao wake. Usishangae kwamba unachokiona wewe kuwa kizuri mwingine hukiona kibaya. Lakini ni kweli kwamba kila mtu hupenda uzuri na ndio maana vioo vinaendelea kuuzwa. Na kwa hiyo nakubali kuwa uzuri ni kitu muhimu katika kuleta furaha.
Mzee akaendelea kueleza kuwa mali ni kitu muhimu pia. Lakini hivi leo si kitu cha kushitua wala kushangaza sana maana watu wengi wanayo na kama mtu akiitafuta kwa bidii ataipata. Kupendwa ni muhimu pia,maana upendo ni tunda la roho;kila mtu
anahitaji kupenda na kupendwa. Lakini pamoja na umuhimu wake si kitu cha kusitua sana maana hata paka ana mkwewe.
Akasema usalama pia ni muhimu kwa mtu kuwa na furaha maana huwezi kuwa na raha kama unajua uko hatarini. Na umaarufu si ajabu mtu kuutamani maana mtu
akiishapata vingine vyote hutamani sana kujulikana na kuwa maarufu.
Baada ya maelezo hayo mzee akachukua kalamu yake nyekundu na kupiga mistari miwili mikubwa ya alama ya X katika karatasi hiyo. Kijana akashituka na kumwangalia mzee kwa mshangao. Mzee akamwambia kijana hivi vitu vyote ulivyoorodhesha ni vya
muhimu sana lakini haviwezi kuwa na maana yoyote katika maisha ya mtu bila ya kuwa na 'amani ya roho' na hiyo haipatikani hovyo wala kununuliwa dukani bali mwenyezi
Mungu huwapa wale aliowaridhia.
Ukweli wa maneno ya mzee huyo mwenye hekima unaonekana kila siku katika maisha yetu. Wapo watu wengi wanaoishi kwa furaha sana pasipo kumiliki mali nyingi, kuwa maarufu au kuwa na vitu tunavyodhani kuwa vya muhimu sana. Kwa upande mwingine wapo mamilionea wengi wanaohangaika kuutafuta usingizi na hata kujiua.
Haishangazi kwamba watu matajiri na maarufu wa Hollywood ndio wanaongoza kwa kupeana talaka. Miaka kadhaa iliyopita mwanamuziki maarufu na mpenda uzuri Michael Jackson alifariki dunia baada ya kuzidiwa na madawa ya usingizi. Ni dhahiri
kwamba bila kuwa na amani ya roho mtu hawezi kuishi maisha ya furaha.
Kumbe tunapojiwekea malengo mengi ya kuyatekeleza katika maisha yetu ni lazima pia tujihoji kwamba malengo hayo yanaelekezwa katika kujipatia nini?
Afya njema?
Mali?
Mapenzi?
Usalama?
au
Umaarufu?
je! tukiishakupata hivyo vyote tutakuwa na furaha? Ni dhahiri kwamba tunavihitaji sana vitu vyote hivyo. Lakini bila amani ya rohoni hatuwezi kupata furaha ya kweli.
Na kwa sababu hiyo swali la msingi linakuwa ni jinsi gani mtu anavyoweza kuipata amani ya roho?
0 comments: