Kwa kila baya ufanyalo tambua unaonekana hata kama ungejificha wapi na mwisho wa siki dhamira hukusuta.

06:24:00 Unknown 0 Comments

Mama mmoja aliyeachwa na watoto wake wawili wakuwazaa pamoja na watatu ambao marehemu mmewe aliwazaa na mama mmoja wa nje ambaye naye alikuwa marehemu, mama alizidiwa sana na homa kali na kuamua kuwaita wanae kwa makundi ili aseme nao na kuwapa urithi.

Alianza kuwaita wale watoto wa mke mwenza na kuwaambia anawapa mali kwa siri ili kila watoto wake wasilifahamu hilo.Akawapa hati ya shamba moja dogo ambalo lilikuwa mbali sana sana na makazi ya watu akitambua kuwa wangeshindwa kuliendeleza na kuwa mwisho wao.

Kisha akawaita wale watoto wake na kuwapa kila aina ya mali zilizosalia na kuwaambia pia kamwe wasiaambie wale watoto na watakapotaka kufungua zile bahasha zenye viambatanishi vya mali hizo wahakikishe wako peke yao ili wale ndugu zao wasiwaone na kuingiwa na wivu na mwishowe kuanza kugombania pia.

Muda mfupi baadae yule mama alifariki, wiki chache baada ya mazishi wale watoto wenye kupewa mali kidogo wakaanza safari ya kwenda kuangalia mali yao waliyopewa na hawa wengine wakabaki pale nyumbani.

Lakini kila walipotaka kukaa wafungue zile bahasha ili wagawane zile mali mioyo yao ikawajaa hofu na kuona kama wanaonekana na kuna baadhi ya ndugu wanawaona hasa wale watoto wengine.

Iliwachukua zaidi ya wiki kadhaa kila wakijaribu walipatwa na mkasa ule ule na wakashindwa cha kufanya, wakaogopa kuwashirikisha ndugu zao na kuamua kwenda kwa mchungaji wao.

Mchungaji baada ya kusimuliwa kisa kile akawauliza swali, " Je kwa uelewa wenu mnafikiri kuna tatizo?" Watoto kwa pamoja wakasema , " Tunafikiri mama alikosea kutupa sisi umiliki mkubwa wa mali zaidi ya wenzetu ambao hata kama sio wa mama huyu ni wa baba yetu na tumekuwa pamoja hivyo nao wana haki"

Mchungaji akawaambia, "Ni kweli mmeongea vyema, kumbuka katika kila baya ufanyalo ambalo ni la dhuluma kwa mwingine lazima utakosa raha, utajiona wewe ni mtu usiye na amani na kama haitoshi utahisi kila mtu anakuona pia"

Watoto walirudi nyumbani wakiwa wamebadilika na kugawana malizi zile upya na wenzao na kwa pamoja wakazisimamia zile mali na kuwa familia yenye furaha, upendo, amani na mafanikio zaidi.

Ni kosa kubwa kupandikiza chuki kwa wanao kwa makosa ambayo wewe na mwenza wako mliyafanya.

Kwa kila baya ufanyalo tambua unaonekana hata kama ungejificha wapi na mwisho wa siki dhamira hukusuta.

Ni wangapi leo waliotumia utajiri wa haramu kuua watu au nduguzo lakini hawana furaha wanakimbia kanisa moja kwenda jingine lakini hawapati amani ya roho?

Kwa kila tufanyacho tujaribu kuamini upendo, amani na furaha kuwa nguzo yako kuu nawe utavuna furaha, upendo na mafanikio ya siyo na kikomo kwa maisha yako yote na hata baada ya kifo vizazi vyako vitayafurahia pia

You Might Also Like

0 comments: