Jumatatu yanikosesha bahati ya kumiliki kitu kizuri
Raia mmoja wa kigeni alikuja Tanzania kufanya kazi katika shirika moja la kujitolea akiwa kama meneja mkuu.Wakati anaondoka akagawa mali zake kwa wafanyakazi wa shirika lile kwa bei nafuu sana sawa na kutoa bure.
Baada ya kugawa vyote akajikuta anapata mtihani mmoja wa kuuza gari lake la kifahari, kwani kuna vijana watatu wote walilitaka na wana bei sawa na yeye hakutaka kuzidisha bei ya gari lile.
Akakaa na kufikiri kisha akaja na jibu na kuwaita wale vijana wote watatu na kuwaambia, " Kwa kuwa wote mnalitaka gari hili basi mimi nitawapa bila kupandisha bei, jumatatu nitakuwa nyumbani kwangu, na wa kwanza kufika saa 11:00 za alfajiri pale nyumbani kwangu atapewa gari"
Wale vijana wakakubaliana nae na kumshukuru na wote wakimhakikishia kuwa bado atakuwa na mtihani mmoja kwani wote watafika muda huo huo.
Jumatatu ile kijana wa kwanza alifika pale saa 11 kasoro na moja kwa moja akaelekea karibu na geti na ilipofika saa kumi na moja kamili akaingia kwa mlinzi na kuonana yule mwenye gari na akampa dokyumentsi na ufunguo wa gari lile na kumwambia fedha amwekee kwenye akaunti yake.
Baaada ya kijana kulikagua gari lake akaliwasha na taratibu akaanza kuondoka akiwa mmiliki halali wa gari lile.
Yule kijana akiwa ndani ya lile gari la kifahari anarudi mijini akakutana na kijana wa pili ikabadidi ampe lifti kabla ya kukutana na kijana wa tatu ambaye nae alikuwa ndio kwanza anajivuta kuliwahi gari huku kashachelewa zaidi ya saa zima.
Nini unajifunza hapa?
Je na sisi ni mara ngapi tumekosa mambo mazuri kwa kutofuata muda?
Kijana wa kwanza yeye jumapili usiku aliweka mambo yake sawa na kupumzika mapema na kujiandaa kwa ahadi ya siku ya pili, lakini kijana wa pili yeye aliamini atatumia uzoefu bila kujiandaa, kijana wa tatu yeye alikunywa pombe huku akitazama mpira bila kuweka utaratibu mzuri wa kuamka mapema na alipokuja kushtuka muda ulishakwenda.
Je hata kama kijana wa pili na watatu wangefanikiwa kulipata gari hilo unafikiri wangekuwa makini kwa kulitunza gari?
Ni vyema kujenga mazoea ya kujali muda, kuthamini mipango yako na kuishi kwa kufuata nini umekipanga kukupata katika maisha.
Sio kazi rahisi kuyafikia maisha unayoyatamani kama hutajali muda, kuwa na heshima ya matumizi ya muda wako na kukijali kile ulichojipangia.
Nakutakia wiki yenye baraka na mafanikio mengi sana na MUNGu azidi kukufungulia milango ya mafanikio kwa kadri unavyojituma na kujali kazi na muda pia.
Kumbuka umepata bahati ya kufanya hicho ulichonacho kwani kuna kundi la watu wanategea wewe ufanikiwe na kuja kuwapa masaada.
Jumatatu njema
0 comments: