Kabla hujaanza kuzunguka na bahasha soma hapa.

14:58:00 Unknown 0 Comments

Miezi michache iliyopita wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wamemaliza mitihani yao ya mwisho wa mwaka. Na kati yao kuna ambao wamemaliza masomo yao ya elimu ya juu. Kwa sasa wengi wanaomaliza wanamaliza kwa ngazi ya shahada(degree). Wanafunzi wanaomaliza elimu ya juu kwa mwaka ni zaidi ya elfu arobaini(40,000). Hivyo kwa miezi miwili iliyopita tayari mtaani kumeingia watu efu arobaini waliohitimu kada mbalimbali. Kama wewe ni mmoja wao ama unaelekea kuwa mmoja wao ni bora ukasoma hapa ili kupata mwanga kidogo.

Wazo kuu ulilonalo kichwani kwa sasa ni kutafuta ajira. Ndio wengi wa waliomaliza wanafikiri kutafuta ajira, sio vibaya kwani ndio ulichosomea. Kama umesomea uhandisi inabidi utafute sehemu ya kufanya huo uhandisi wako, kadhalika kwa kada nyingine. Wakati mkiwa chuoni kulikuwa na habari nyingi kuhusiana na ajira za kada uliyosomea ikiwemo upatikanaji wake na pia mishahara ya ajira hizo. Kuna baadhi ya habari ulizokuwa unasikia ni za kweli ila nyingi zilikuwa sio sahihi sana. Kwa kuwa sasa umeingia mtaani utauona ukweli wenyewe kwa vitendo na sio nadharia tena.

Kuna uwezekano umeshaandaa vyeti vyako na wasifu wako na upo kwenye michakato ya kuanza kuzunguka na bahasha kupeleka sehemu mbalimbali ii kuomba nafasi ya ajira. Kabla hujaweka nguvu na matumaini yako kwenye mchakato wa kuzunguka na bahasha kuna vitu vichache ambavyo ni vyema ukavijua.

1. Nafasi za ajira ni chache kuliko idadi ya wahitimu na wenye sifa. Kwa sasa karibu kila kada ukiondoa elimu na afya kuna nafasi chache sana serikalini na hata kwenye taasisi binafsi. Hata kwa kada ya elimu nako kwa miaka ya hivi karibuni kuna baadhi ya wahitimu wamekosa nafasi za kazi. Hivyo unavyoingia sokoni jua kabisa ‘demand’ ni ndogo kuliko ‘supply’

2. Sio kila nafasi za kazi zinazotangazwa ziko wazi. Kuna baadhi ya taasisi zinatangaza nafasi za kazi ili tu kutimiza wajibu na sheria ya kutaka ajira zitangazwe kwa umma. Hivyo unaweza kuandika maombi, ukaitwa kwenye usaili na bado ukaambiwa umekosa nafasi.

3. Wenzako wa mwaka jana na mwaka juzi bado wanazunguka na bahasha. Bado kuna wahitimu wengi wa miaka iliyopita nao bado hawajapata ajira. Kuna ambao bado wanaendelea kupitisha bahasha na kuna baadhi ambao wameamua kufanya mambo mengine. ni vyema kuwatafuta wa kila kundi ili ujifunze machache kutoka kwao.

4. Mishahara ya kazi za kwenye taasisi binafsi ni midogo sana. Tofauti na story za vyuoni kwamba mishahara inaanzia labda laki tano au laki saba jua kuna wenzako wana degree hivyo hivyo na wanalipwa laki mbili. Kama ukipata kazi na mshahara wakakutajia mdogo kama huna kingine cha kufanya ni bora kuchukua kazi hiyo ila uifanye kwa lengo la kupata ujuzi na kujenga mtandao na watu wanaofanya kada uliyosomea. Kuliko kukaa mwaka mzima ukizunguka na bahasha ukitegemea mshahara mkubwa ni bora kupata japo laki mbili kwa mwezi huku ukiendelea kukuza mtandao wako na ujuzi wako.

5. Kuna kazi za kujitolea, kama umekosa hata kazi ya bei rahisi kuna taasisi nyingi ambazo zina mpango wa watu kujitolea kufanya kazi na baadae unaweza kuingizwa kwenye ajira. Kama hali ya nyumbani inaruhusu kwa kuweza kupata kula na nauli fanya kazi za kujitolea na huko onesha uwezo wako na vipaji vyako. Kwa kuonesha uwezo na vipaji ni rahisi sana kukubalika na kupewa nafasi, na pia utatengeneza mtandao wa watu watakaokuonesha njia zaidi.

6. Sio lazima ufanye kazi ya kitu ulichosomea. Kuna baadhi ya kazi zinaweza kufanywa na mtu yeyote aliehitimu elimu fulani. Kwa mfano kwa sasa kuna uhaba mkubwa wa walimu, hivyo kama umehitimu unaweza kutafuta shule na ukafundisha masomo yanayohusiana na ulichosomea. Kama umesoma kada za biashara unaweza kufundisha masomo ya biashara, kama umesoma sayansi kuna nafasi kubwa za kufundisha masomo ya sayansi kutokana na uhaba wa waalimu wa sayansi. Kama unadhani kushika chaki sio hadhi yako basi endelea kuzunguka na bahasha mjini.

7. Angalia mazingira yanayokuzunguka na jinsi unavyoweza kuyatumia kutengeneza ajira kwako na kwa wanaokuzunguka. Hii ndio dhana halisi ya elimu ila kwa kuwa elimu yetu inatuandaa kuwa waajiriwa basi tunajikuta wote tunasubiri kuajiriwa.Ni vyema ukaanza kufikiri tofauti na uliyofundishwa chuoni kuhusu ajira.

8. Cha mwisho kabisa ambacho ni vyema ukakijua na ambacho ingebidi kiwe cha kwanza ni kufanya maamuzi ya kujiajiri. Kama utachoshwa na kuzungusha bahasha ama kama hutaki kupata hiyo karaha ni vyema ukafanya maamuzi ya kutotegemea kuajiriwa. Tumia uwezo na vipaji ulivyonavyo changanya na elimu uliyoipata halafu tumia mazingira uliyopo kutengeneza ajira kwako na kwa wanaokuzunguka.

You Might Also Like

0 comments: