MATAPELI WANAVYOIBA KUPITIA MAHAUSIGELI

10:09:00 Unknown 0 Comments

UKIWA una dhahabu, yaani hereni, mikufu, pete ama bangili za dhahabu basi unatakiwa kusoma mkasa huu ili ukampe somo ‘hausigeli’ wako na achukuwe tahadhari atakapokutana na matapeli ambao hupenda kuwachota akili na hatimaye kujikuta mkiibiwa.
Matapeli wa madini mara nyingi hutumia akili sana kukuibia. Hufanya utafiti na kujua nani katika mtaa fulani ana  mkufu, hereni, pete au bangili za dhahabu.
Kabla ya kukuibia atataka kujua je, huwa inazivaa wakati wote? Akijua kuwa huwa una kawaida ya kuvua dhahabu hizo, hufanya utafiti kwamba huwa unaziweka wapi katika nyumba yako. Kabatini au sandukuni.
Wenyewe wana njia zao za kupata habari hizo ama kwa kutumia ‘mahausiboi’ au mahausigeli au ndugu zako unaoishi nao ambao bado siyo wajanja wa mambo ya mjini.
Akishapa taarifa hizo na kujiridhisha huingia kazini. Soma mkasa huu utajifunza kitu.
Siku moja hausigeli mmoja aliachiwa fedha za kununua mafuta ya taa katika Sheli ya Bamaga, Mwenge jijini Dar na mama mwenye nyumba wake. Aliambiwa anunue mafuta hayo ya taa lita tano.
Kwa kuwa kutoka nyumbani hadi sheli ya Bamaga siyo mbali (Alikuwa akiishi Mwenye kijijini), aliamua kuchukua galoni lake la lita tano na kwenda kununua mafuta ya taa.
Ilikuwa kama saa tano hivi. Kabla ya kufika sheli alikutana na mvulana mmoja mwenye umri wa miaka kama 28 au 30 hivi na akamsimamisha.
“Dada samahani. Una bahati mbaya sana,” alisema yule mvulana.
“Kwani nina nini?” alihoji hausigeli.
“Una bahati sana kukutana na mimi kwani mimi ninakwenda pale Chuo Cha Ustawi wa Jamii, kuna msichana mmoja jana alikuwa na tatizo, nikamsaidia na leo nakwenda kumpa mzigo wake.”
“Huyo msichana alikuwa na nini?”
“Tatizo lake ni kama lako.”
“Lipi?”
“Hebu funua mdomo.”
Yule hausigeli alifunua mdomo na yule kijana akaanza kutoa unywele mrefu sana, mpaka msichana akaanza kuogopa na kutokwa jasho.
Baadaye ule unywele ukawekwa kiganjani na kabla hajasema chochote akatokea kijana mwingine, (mwizi mwenzake), akajifanya kama ametaharuki.
“Mtaalamu nashukuru kukuona, unajua siku ile umemuokoa dada yangu kwa kile kitendo cha kumtoa unywele kinywani, nakushukuru sana. Hukunitoza chochote na ilikuwa tukutane ile sehemu leo jioni, maadamu nimekutana hapa, chukua hizi shilingi laki moja kama shukrani yangu. Wewe mtu mzuri sana.”
Baada ya mtu yule kusema hayo alitoa shilingi laki moja akampa na wakaagana na akaondoka na kuwaacha yule ‘mtaalamu’ na hausigeli.
Yule mtaalamu mwizi akamwambia hausigeli kuwa huwa hatozi fedha kwa watu anaowaokoa kama alivyojionea yule mtu aliyempa zawadi.
Alimwambia kuwa kwa tatizo lake dawa pekee ambayo itamfanya asife siku mbili zijazo ni kwenda kuchukua dhahabu za mama mwenye nyumba wake na akizileta zitachanganywa na dawa ambayo atainywa, na dhahabu kurudisha alipoitoa, hivyo kuokoa maisha yake.
Alimwambia anajua kuwa dhahabu hizo zipo kabatini chumbani kwa mama mwenye nyumba yake, hivyo aende kuzichukua na hilo asimuambia yeyote mpaka dawa ifanywe la sivyo atakufa ghafla akianza kutamka tu hayo.
Hausigeli alichanganyikiwa akaenda nyumbani na moja kwa moja chumbani kwa mama mwenye nyumba wake ambaye hereni, mkufu na bangili zake za dhahabu huzivaa wakati wa hafla maalum tu na kuziweka kwenye mkebe kabatini, akafungua kabati na kuchomoka na mkebe ule.
Alipomfikishia mkebe ‘mtaalamu’ mwizi, aliufungua na kumwambia auweke kwenye ‘brifkesi’ yake, akafungua mkebe wa dhahabu na kubadilisha, akamuwekea dhahabu feki bila hausigeli kujua.
Alimpa masharti kwamba asiufungue hadi atakapofika nyumbani na kabla ya kuuweka sehemu aliyoukuta aufungue na kupulizia dhahabu na kesho yake wakutane palepale ili ampe dawa ya mwisho.
Yule hausigeli alirudi nyumbani lakini alipofungua mkebe wa dhahabu ili apulizie kama alivyoelekezwa, aligundua kuwa ameibiwa kwa sababu alikuta mkufu wa dhahabu feki na bangili na hereni hakuna!
Alianza kulia hadi mama mwenye nyumba alipofika saa kumi jioni.
“Wewe msichana unaumwa?” aliuliza mama mwenye nyumba.
Hakujibiwa.
“Si nakuuliza? Unaumwa nini mbona unalia?”
“Mama samahani sana, nime…. Nime…nimeee,” alishikwa na kigugumizi.
“Umefanyaje” Sema, unanitia presha.”
“Mama nimeibiwa.”
“Umeibiwa nini?”
“Dhahabu zako kuna mtu nimempa, kaniibia mama yangueee?”alianza kulia kwa sauti hadi majirani wakajaa tele pale nyumbani.
“Umempa kijana gani na kwa nini umeingia chumbani kwangu na kuchukua mkebe wenye dhahabu zangu we msichana?”
Ilibidi asimulie mkasa mzima tangu mwanzo hadi mwisho.
 Mama mwenye nyumba hasira zilimshika na akabaini kuwa ni kweli ameibiwa dhahabu zake zote ambazo thamani yake zilikuwa ni zaidi ya shilingi milioni mbili!
Ushauri wangu kwa akina mama na hata akina baba walio na wasaidizi majumbani mwao kuwaelimisha kuwa wasikubali kurubuniwa na mtu yeyote kutoka kifaa chochote ndani ya nyumba.
Huyu katoa dhahabu, wengine wanaweza kuja na staili nyingine ilimradi tu afanikiwe kuiba. Wito kwa mahausigeli pia kwamba ukikutana na mtu ambaye humjui usikubali kuongea naye chochote kwa sababu huyo anaweza kuwa mwizi kama mtaalamu huyu feki.

Source: GPL

You Might Also Like

0 comments: