Kombe la dunia ni kipimo tosha cha kuonyesha mabadiliko ya kasi ya kimaendeleo .....Nawe waweza jipima
Kombe la Dunia la FIFA ni kipimo kingine cha jinsi dunia inavyobadilika kwa kasi sana.
Michuano ya 1990 nchini Italia na ile ya 1994 nchini Marekani, kwa nchi za dunia ya tatu kama Tanzania, redio ndo ilikuwa chanzo
kikubwa cha habari kwa watu wengi. Watu
wengi walipata taarifa kupitia chombo hicho. Ilipofikia 1998 michuano ilipofanyika Ufaransa,
watu wengi waliweza kupata habari kwa kupitia runinga.
Ilipofikia 2002, michuano ikafanyika Japan na Korea. Ukiachilia mbali runinga, huduma ya ujumbe mfupi wa maandishi (sms) ilikuwa njia
muhimu ya watu kubadilishana habari kuhusiana na michuano hiyo.
Mwaka 2006 wakati michuano hiyo ikifanyika nchini Ujerumani, ukiachilia mbali runinga na sms, internet ilikuwa chanzo kingine kikubwa cha habari.....hapo ndipo Yahoo Messenger, Dar Hotwire na kadhalika zilikuwa kwenye chati sana.
Mwaka 2010 Afrika ikaeneza shangwe dunia nzima kutoka Afrika Kusini. Runinga zilishakuwa kitu cha kawaida sana. Watu wengi
walitazamia michuano kutoka masebuleni kwao.
Ushabiki wa mpira wa miguu
ukaongezeka kwa kasi mno. Moja ya vichocheo vikubwa vya kuongezeka kwa ushabiki ni kuja kwa mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter. Facebook na Twitter vikashika kasi
kama vyanzo vikubwa vya habari za kandanda tena kuliko hata runinga. Maana, mtu yeyote aliyekuwa na simu yenye internet aliweza
kufahamu kinachojiri kutoka pahala popote alipo. Pia, tukaanza kuwa na uwezo wa kuyaona magoli na highlights zingine kupitia YouTube na kadhalika.
Sasa ni 2014, kandanda linasukumwa kutoka nchini Brazil huko Amerika ya Kilatini. Runinga
bwerere. Mitandao ya kijamii imezidi kushika kasi. Sasa, ukiachilia mbali Facebook na Twitter, kuna ndugu yao aitwaye WhatsApp.
Huko nako taarika za kandanda zinaenea kwa kasi mno kupitia makundi mbali mbali yaliyoundwa kwa malengo kadha wa kadha, na
kwa kupitia mtu mmoja mmoja.
Kuna applications kama Livescore, Google Now na kadhalika ambazo zinakujuza kila dakika inayoyoma uwanjani. Sasa mtu hapitwi na
jambo.
Kweli dunia inabadilika kwa kasi mno. Hatufahamu, mwaka 2018 michuano hii itakapokuwa ikifanyika nchini Urusi na 2022
huko Qatar, maendeleo ya dunia hii yatakuwa yamefikia kiwango kipi.
Ama kweli, kila zama na mambo yake. Na kila mambo na upekee wake.
Fadhy Mtanga ,
Mbeya.
Jumamosi, Julai 5, 2014.
0 comments: