UNATAKA NDOA ISIYO NA MGOGORO KABISA? BASI USIOE AU KUOLEWA MAANA HAIPO KABISA

13:31:00 Unknown 0 Comments

Kabla sijaingia kwenye mada ya leo kama inavyosomeka hapo juu, napenda kuwashukuru wasomaji wangu ambao wamekuwa wakinipigia simu kila mara kutokana na kuguswa na mada ya wiki iliyopita, Ahsanteni sana na Mungu azidi kuwabariki.

Matatizo ni sehemu ya maisha na  ndoa ni sehemu ya maisha, elewa kuwa utakuwa na mikwaruzo ya hapa na pale, cha msingi ni kujua namna ya kusuluhisha kasoro hizo, hatimaye muweze kwenda sawa na mwandani wako.

Siri moja ya msingi kabisa katika maisha ya ndoa ni kuhakikisha kila mmoja wenu anamsoma mwenzake  na kujua  udhaifu na uimara wake.

Kuingia kwenye ndoa ni jambo zuri, lakini unatakiwa kuwa makini na aina ya mtu ambaye unamchagua ili awe mume au mkeo, kwa sababu si kila mtu anafaa kuishi katika maisha ya ndoa. Zingatia sana.

Kwa nini hakuna ndoa isiyo na migogoro hata kidogo? Nini kinashindikana kuwa na ndoa yenye amani siku zote? Si mnapendana kabisa? Ugumu uko wapi? Hapa chini kuna sababu ambazo zinachangia kutokuwepo na ndoa isiyokuwa na migogoro hata kidogo.

ASILI YA KILA MOJA
Kila binadamu ana asili yake ambayo ni tofauti na mwingine. Uchoyo, uchafu, hasira na uropokaji ni mifano ya asili ya kibinadamu. Japo katika maandiko matakatifu tunajifunza kuwa asili yetu sote ni kwa Adamu kama binadamu wa kwanza kuumbwa na Mungu (Imani ya kidini), ni ukweli usiopingika kuwa tunatofautiana kwa mambo mengi.

 Hapa naingia moja kwa moja katika asili ya makabila, mila, miiko na desturi ambazo tunakutana nazo katika makuzi tunayopitia kabla ya maisha ya ndoa na jinsi ambavyo huchangia migogoro katika ndoa.

Sasa unakuta kila moja wenu amefundishwa maadili tofauti juu ya kitu fulani, mfano labda katika kabila fulani ni mwiko kabisa kuongea wakati wa kula, au hairuhusiwi  mwanamke kula kichwa cha samaki, pengine ni marufuku kulala ukiwa mtupu. Sasa kwa mila na miiko hiyo, unakuta ni tofauti kabisa na ya mwenzako.

Tofauti hizo za kiasili ndizo unakuta zinachangia migogoro ya hapa na pale maana kila mmoja wenu anakuwa na asili tofauti ya mila na desturi pamoja na miiko. Hivyo basi, ni lazima kuna mahali mtatofautiana tu na ndiyo maana nikasema kuwa hakuna ndoa isiyokuwa na migogoro hata kidogo. 

Sasa umeona jinsi tofauti za asili zinavyoweza kuleta migogoro? Basi tuingie kwenye sababu ya pili.

FAMILIA
Katika familia kuna malezi na mafunzo mbalimbali yanayotofautiana kutoka moja hadi nyingine. Hapa ndipo kwenye msingi mkubwa kabisa katika kipengele cha kuwa na mwenzi sahihi wa maisha. 

Malezi ya familia huchangia mtu kukua katika msingi bora wa maisha au kutokuwa na maadili mema,  ndiyo maana ukikuta mtu ana tabia mbaya katika jamii, basi watu huanza kuuliza hivi huyu amelelewa katika familia ipi? Hata zamani mtu akitaka kuoa au kuolewa, jambo la kwanza kabisa ni kuchunguza familia ambayo mwenzi wake anatoka na wakati mwingine uchumba ulikuwa unakufa kabisa kutokana na utofauti wa malezi na misingi ya familia.

Kwa hiyo mkiwa katika ndoa, migogoro mingine hujitokeza kutokana tu na tofauti ya malezi na maadili ya kifamilia. Mathalani katika familia yenu wewe mwanamke, mlikuwa na mazoea ya kula chakula cha mchana saa 8 mchana na cha usiku saa 3, sasa unakuta hali ni tofauti kabisa na familia ya mume wako ambayo ilikuwa na kanuni ya kula saa 6 na saa 2, tayari hapo kunakuwa na  mgongano fulani ambao msipouwahi unaweza kuwa ni tatizo.

Kwa hiyo tofauti ya malezi ya kifamilia, huchangia kuibuka kwa matatizo ya hapa  na pale katika ndoa nyingi  hasa pale mnapokuwa na watoto maana kila mmoja wenu atajaribu kuingiza malezi aliyofudishwa katika familia yake na mwenzako anaweza kuyaona hayafai na ni upotoshaji wa maadili. Kinachofuata hapo ni mabishano na migogoro kama siyo mitafaruku.

MAZINGIRA
Kabla ya kuishi katika ndoa, tunapitia mazingira tofauti kila mmoja wetu kwa mfano  shuleni, mitaani na hata nyumbani  ambapo unakutana na aina tofauti ya kuishi  kama  ulivyofundishwa na wazazi wako.

Aina ya watu ambao unakutana nao katika kipindi cha kuingia katika utu uzima ndiyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu au kutengeneza maadili ya ukuaji wa mtu.

Aidha, kabla na baada ya kuoa au kuolewa  mazingira unayokutananayo yanaweza kukuharibu na kukusababishia matatizo katika ndoa.
Wiki ijayo, nitaeleza sababu  zinazochangia kutokuwepo na ndoa isiyokuwa na migogoro kabisa, usikose nakala yako.




You Might Also Like

0 comments: